LAITI
Shairi
Si huku, si huko – wapi sikuranda, nikayumba…
Lipi sikutenda – kwa wingi wa mashobo
Na kichwa kigumu na sikio lisilosikia dawa
Wala la mwadhini
Mama kasema lipi? Mwalimu je?
Sayari ya athi ikanipeleka chuo
Chuo kilichokosa mwelekeo – kikanipepesa na kunirusha ovyo.
Na baba…
Laiti angalikuwa hai,
Angalinionyesha tariki,
Angaliniambia ukweli,
Ukweli ninaougundua kwa uchungu mwingi.
Kuwa mtima, mdanganyifu – nisiuamini katu.
Kuwa maisha mlima, nisiyaparamie kwa pupa
Pupa ambayo imenitongoza kupenda
Visivyotamanika.
Ningalipunguza uguo la moyo
Fundo chungu lililokatalia kooni, limekaa sawia
Nisingaliweka ya chemba wazi, penye fisi
Wanaobeua na wingi bughudha
Angaliniambia, ‘mwanangu nakupenda’
Hilo lingenipa mtizamo.
Ningalijua pakuelekea, pakuegemea hata pakuepuka
Nisingalichafua hiki kitabu kwa machozi na wino
Humu gizani, giza totoro la jela.
Written on July 4, 2017 and first draft appeared on poetryfolks